Mahakama ya Juu Kenya yashindwa kusikiliza kesi ya kuahirishwa kwa uchaguzi kutokana na ukosefu wa majaji wa kutosha mahakamani.
Jaji Mkuu David Maraga amesema baadhi ya majaji wamo nje ya nchi na wengine hawangeweza kufika mahakamani kwa sababu mbalimbali.
Kesi hiyo ilikuwa imewasilishwa na wapiga kura watatu wakisema Tume ya Uchaguzi haiko tayari kuandaa uchaguzi huru na wa haki kesho.
Jaji Mkuu amekuwa mahakamani na Jaji Isaac Lenaola pekee.
Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu hakuweza kufika kortini baada ya kupigwa risasi kwa dereva wake jana jioni.
Jaji Ibrahim, ambaye amekuwa akiugua, yuko nje ya nchi.
Majaji Smokin Wanjala na Jacktone Ojwang hawakuweza kufika kortini pia.
Jaji Njoki Ndung'u alikuwa amesafiri nje ya jiji la Nairobi na hakuweza kupata usafiri wa kumuwezesha kufika mahakamani kwa wakati.
"Sisi wawili hatuwezi kufikisha idadi inayohitajika ya majaji mahakamani kwa mujibu wa kifungu 162 (2) cha Katiba. Kesi imeahirishwa hadi wakati mwingine," ametangaza Jaji Maraga.
Kifungu hicho cha Katiba kinasema kikao cha mahakama hiyo kinafaa kuwa na majaji angalao watano.
Wakili wa raia hao watatu waliokuwa wamewasilisha kesi hiyo, Harun Ndubi, ameshutumu hatua ya majaji kukosa kufika kortini akisema ni jambo la kushangaza.
"Wakitoweka wakati tunawahitaji kutekeleza jukumu hili muhimu, unashangaa iwapo wanafuata kiapo walichokula," amesema.
Seneta wa Siaya James Orengo aliyewakilisha Raila Odinga mahakamani wakati wa kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa tarehe 8 Agosti amesema kilichotokea leo ni "mapinduzi ya katiba".
"Haya yamekuwa yakifanyika, hata katika tume ya uchaguzi. Stakadhabi zilizowasilishwa na tume kujibu kesi zimewasilishwa na naibu mwenyekiti na wala si mwenyekiti. Ni wazi kwamba tume ya uchaguzi inafanya kazi bila mchango wa mwenyekiti. Wafula Chebukati amekuwa abiria," amesema.
"Taasisi ambayo imelemazwa na Jubilee kwanza ni IEBC. Na tume iliyosalia haina uwezo wa kuandaa uchaguzi."
Bw Orengo amesema anaamini ukosefu wa majaji wa kutosha mahakamani haufai kushangaza wengi na kudokeza kwamba uamuzi wa kutangaza leo kuwa Siku ya Mapumziko ulilenga kuvuruga shughuli za mahakama.
"Kuna jaribio la kuhujumu taasisi za serikali zikiwemo taasisi huru kama vile tume ya uchaguzi na Mahakama ya Juu," amesema.
Post a Comment