MWEZI mtukufu wa Ramadhani umegawanyika katika makundi matatu ambayo yana siku kumi kila moja, na kila kundi moja la kumi lina faida zake kwa mwenye kutimiza kile kilichoagizwa na Mwenyezi Mungu.
Kumi la kwanza linajulikana kwa jina la Rehma (rehema), la pili Magh-fira (kusamehewa madhambi) na lile la mwisho linaitwa kumi la kuachwa huru na moto.
Katika kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani vitu vinavyopaswa kufanywa zaidi ni kuswali, kutoa zaka na matendo mengine ambayo kwa kiasi kikubwa humpwekesha Mwenyezi Mungu.
Katika mwezi huu, kila jema analofanya mja hulipwa zaidi kuliko ambavyo analipwa katika siku za kawaida, ndiyo maana watu hufurika kwa wingi katika nyumba za ibada.
Kumi la Rehma hupata baraka na kwa kila nachokifanya huku shetani akifungwa minyororo ili asiweze kuwarubuni watu.
Mtu mwenye kutimiza yale yanayotakiwa katika kumi hili, hupata thawabu nyingi pamoja na kujifungulia milango ya kuingia katika kumi la pili ambalo ni Magh-fira.
Wanazuoni na hadithi mbalimbali zinatanabaisha kuwa, mtu mwenye kufanya ibada na kusoma kitabu kitukufu cha Qur-an katika mwezi huu, husamehewa dhambi zake zote alizozitenda huko nyuma.
Kumi la mwisho ni la kuachwa huru na moto, ambapo waja ambao wametenda mema katika makumi yaliyotangulia, huondolewa adhabu zote zilizokuwa zikimkabili siku ya kiama.
Katika kumi hili la mwisho, Waislamu hutakiwa kukesha zaidi katika nyumba za ibada kwa kuwa ndipo hupatikana usiku mtukufu ambapo kitabu cha Qur-an kilishushwa (Laila-tul Kadir)
Kwa mujibu wa vitabu mbalimbali vya dini Malaika hushuka ardhini kutafuta watu wenye kusoma Qur-an au kufanya ibada mbalimbali ambazo humpwekesha Mwenyezi Mungu.
Mja yeyote ambaye Malaika wakimkuta akifanya ibada na kusoma Qur-an, huwa mwenye kupata daraja ya juu kwa Mwenyezi Mungu pamoja na kufunguliwa mambo yake mengi ambayo yalikuwa yamekwazika.
Kimsingi mwezi huu ni wa mchumo kwa mja, kwa kuwa kila jambo jema analolifanya hulipwa maradufu (thawabu) na kwa mwenye kufanya maasi hakika atakuwa ni mtu mwenye kula hasara mbele ya Mungu na anakabiliwa na adhabu kubwa siku ya kiama.
Mwezi huu ni kama chuo cha mafunzo ambapo baada ya kumalizika, waumini wanapaswa wawe wameelimika na kubadilika ili wawe kama wamezaliwa upya kutokana na kutakasika na maovu.
Haitarajiwi hata kidogo kwa ambaye amejinyima kula (amefunga), kufanya ibada, kusoma Qur-an na mambo mengine mema, kuanza kufanya maasi mara baada ya kumalizika kwa mwezi huu.
Imekuwa desturi kwa baadhi ya Waislamu kuuthamini na kuuona mwezi mtukufu wa Ramadhani ndiyo pekee wa kumuabudu Mwenyezi Mungu na kufanya amali njema huku wakiiona miezi mingine kama wamehalalishiwa kufanya maasi.
Dhana hii inapaswa kuachwa kwa kuwa haitakuwa na maana kama muumini aliyepita katika chuo cha mafunzo (Ramadhani) akalingana au kumzidi yule asiyepitia katika chuo hicho.
Mwenye kurejea kufanya maasi mara baada ya Ramadhani, atakuwa ni sawa na mtu aliyejisafisha vizuri na kuvaa nguo nyeupe, kisha akajirusha kwenye matope.
Kila kitu hujengwa na misingi, mihimili au nguzo zinazokifanya kusimama imara. Mathalani, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inajengwa na mihimili mikuu mitatu, Utawala, Bunge na Mahakama ambavyo aghalabu vyote hufanya kazi kwa kutegemeana.
Misingi ya Kiislamu, nayo hujengwa na nguzo kuu tano ambazo kwanza ni kushuhudia kuwa na imani kuwa hapana Mola anayepaswa kuabudiwa kwa haki isipokuwa Mwenyezi Mungu mmoja na kwamba Mtume Muhammad (Rehema na amani zimfikie) ni mjumbe wa Mwenyezi Mungu.
Nguzo ya pili ni kusimamisha swala tano kwa maana ya kudumu kutekeleza ibada hiyo, yaani Adhuhuri (saa 7 mchana), Alasiri (saa 10 alasiri), Magharibi (saa 12 jioni), Insha (saa 2 usiku) na Alfajiri (saa 11 alfajiri) na ya tatu ni kutoa zaka kwa wenye uwezo.
Mihimili mingine miwili ya Uislamu baada ya Shahada, Swala na Zaka ni kufunga Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, nguzo ambayo ndiyo kiini cha makala hii, na ya mwisho ni Hijja, ambapo waumini wenye kuweza wanakwenda kuhiji katika nyumba ya Mwenyezi Mungu huko Makkah, Saudi Arabia
JIUNGE NASI , BONYEZA HAPA http://www.wabunifumedia.blogspot.com ku-install App ya wabunifumedia, bila ya kuingia website
Tweet@wabunifumediaonline, youtube@wabunifumediaonline TV, Fb@wabunifumediaonline, insta@wabunifumediaonline
.
Tweet@wabunifumediaonline, youtube@wabunifumediaonline TV, Fb@wabunifumediaonline, insta@wabunifumediaonline
.
Post a Comment