Na Issa Ramadhani
INGAWAJE swala la kulea Wazee limeonekana ni mzigo kwa Taifa letu licha ya huduma wanazopatiwa kuwa duni, lakini awamu ya nne ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli, ameamua kulivalia njuga jambo hili na kulipa uzito wa hali ya juu baada ya kutoa agizo kuwepo na utaratibu mzuri wa kukarabati majengo ya Wazee ikiwa ni pamoja na kughakikisha watu hao wanapatiwa huduma bora yenye kukidhi mahitaji yao.
Jambo hilo limeanza kutekelezwa Mkoani Morogoro, baada ya Serikali ya mkoa huo wa Morogoro kutenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa mabati 200 yatakayotumika kuboresha majengo machakavu yaliyopo katika kambi ya wazee na watu wenye mahitaji maalumu ya Chazi, wilaya ya Mvomero pamoja na Funga Funga katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Hatua hiyo imelenga kuwaondolea kero wazee zilizo kuwa zinawakabili kwa takribani muda mrefu huku wakiwa na lengo la kuwahudumia watu wenye mahitaji maalumu wanaoishi kwenye kambi hizo, kutokana na majengo yao kuchakaa yakiwemo mabati ambayo yako katika hali isiyo nzuri na inayoweza kuhatarisha maisha yao.
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Morogoro, Mkuu wa Mkoa huo, Dk Stephen Kebwe, alisema hayo wilayani hapa, kabla ya kumkaribsha mke wa Rais, Janeth Magufuli kuzungumza na wazee wa kambi ya Chazi, iliyopo tarafa ya Turiani, wilayani humu, sambamba na kukabidhi zawadi ya vyakula mbalimbali kwa wazee hao.
Mke wa Rais aliwabidhi wazee na watu wenye mahitaji maalumu wanaoishi katika kambi hiyo vyakula vya aina mbalimbali ukiwemo mchele kilo 875, unga wa sembe kilo 875, sukari kilo 175, maharagwe kilo 350 na mafuta ya watu wenye ulemavu wa ngozi boksi moja.
Kwa mujibu wa Dk Kebwe, pamoja na kambi hizo kuwa chini ya Wizara ya Afya , Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Serikali ya mkoa ina wajibu wa kusaidia kuboresha makazi ya wazee hao ili waone ni nyumbani kwao katika maisha yao ya kila siku.
“Kazi ya kwanza ni kutoa bati katika kambi hizo mbili za Chazi pamoja na Funga Funga, ambapo kila moja itapatiwa bati 100,” alisema Kabwe.
Aidha, Dkt Kabwe, Alisema lengo la ujenzi huo wa kambi za Wazee ni kuzifanya kambi za wazee hao ziwe nuru ya maisha bora.
Hata hivyo, Dkt Kabwe, Alisema tathmini imeanza kufanyika ili kupata gharama halisi za ukarabati wa majengo, uingizwaji wa umeme na upatikanaji wa huduma ya maji.
JIUNGE NASI , BONYEZA HAPA http://www.wabunifumedia.blogspot.com ku-install App ya wabunifumedia, bila ya kuingia websiteTweet@wabunifumediaonline, youtube@wabunifumediaonline TV, Fb@wabunifumediaonline, insta@wabunifumediaonline
Post a Comment