Na Issa Ramadhani
WAKATI Serikali imezuia baadhi ya vyuo vya elimu ya juu kudahili wanafunzi kwa mwaka wa masomo wa 2016/2017, kasoro zilizosababisha zuio hilo zimebainika.
Uchunguzi uliofanywa kwa takribani wiki mbili, ulibaini baadhi ya vyuo nchini hutoa elimu bila ya kuzingatia sifa, huku baadhi vikiwa na idadi kubwa ya wanafunzi kuliko walimu, kutokuwa na maabara na majengo muhimu, kuwa na wanafunzi wasio na sifa, kuwa na wakuu au makamu wakuu wasio na sifa.
Ofisa wa TCU ,Edward Mkaku |
Ofisa Uhusiano wa Tume ya Vyuo Vikuu (TCU), Edward Mkaku, aliliambia gazeti hili siku chache zilizopita kuwa serikali kupitia TCU ilikuwa imeunda Tume Maalum ili kuchunguza uendeshaji wa vyuo vikuu nchini.
Alisema mara baada ya tume hiyo kukamilisha kazi yake, TCU itakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kueleza kile kilichobainika katika ukaguzi huo na hatua zitakazochukuliwa na serikali.
Jana gazeti hili lilimtafuta Mkaku ili kutoa ripoti kamili ya kile kilichobainika ikiwa ni pamoja na kutaja idadi kamili ya vyuo vilivyozuiwa baada ya vyuo sita kudaiwa kusitishiwa udahili wiki iliyopita huku jana kukiwa na taarifa ya vyuo zaidi kuongezeka katika mkumbo huo.
Hata hivyo Mkaku alisema, asingeweza kufanya hivyo kwa sababu alikuwa katika mapumziko na kwamba taratibu za kazi hazimruhusu kufanya kazi siku ya Jumapili.
“Nitafute kesho asubuhi (leo) nitakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kusema kile kilichobainika katika ukaguzi huo na kukutajia vyuo vyote husika. Kwa leo nipo na familia yangu napumzika kwa hiyo nisingependa kuzungumzia masuala ya kikazi,” alisema Mkaku.
Pamoja na utaratibu mpya wa udahili wa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu kupitia TCU kwa wale wanaotoka shuleni moja kwa moja na waombaji wenye astashahada na stashahada ya juu kupitia Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE), serikali iliamua kuunda tume hiyo ili kujiridhisha kuhusu hali ya utoaji elimu ilivyo katika vyuo hivyo.
Gazeti hili lilipata taarifa za mapema kwa Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba na Teknolojia (IMTU) cha jijini Dar es Salaam kuendesha shughuli zake za utoaji wa elimu ya juu huku kikikiuka taratibu mbalimbali lakini lilipotaka kubaini ukweli juu ya taarifa hizo, Meneja Uendeshaji wa chuo hicho, Mathews Diwiz alikanusha madai hayo.
Taarifa za awali zilisema pamoja na mambo mengine chuo hicho kilikuwa kikikabiliwa na uhaba wa wahadhiri wenye sifa kwa muda mrefu na kufanya wahadhiri kufundisha idadi kubwa ya wanafunzi hatua iliyokuwa inasababisha kuzalishwa kwa wahitimu wasio na sifa ya kutosha katika taaluma ya udaktari.
Zilisema pia Mkuu wa Chuo, Issac Umepethy na Makamu wake Dk Naidv Kature, hawakuwa na sifa za kuweza kushika nafasi zao hatua ambayo pia ilikuwa inakifanya chuo hicho kushindwa kujiendesha inavyotakiwa na kuathiri utolewaji wa elimu.
Ilidaiwa pia kuwa pamoja na kutoa mafunzo ya udaktari, chuo hicho hakikuwa na maabara za kutosha, hatua iliyokuwa inakwamisha utolewaji wa mafunzo kwa vitendo na hivyo kuzalishwa kwa madaktari na wataalamu wa afya wenye kiwango kidogo cha utaalamu.
Akijibu tuhuma hizo, Diwiz na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Wanachuo wa IMTU aliyemaliza muda wake juzi, Adili Msika, walisema kwa wakati tofauti kuwa changamoto hizo zilikuwepo awali lakini zilikuwa zimechukuliwa hatua mbalimbali ili kuweza kuzitatua na kwamba hali kwa sasa ni nzuri.
Siku chache kabla ya kutolewa taarifa za chuo hicho kuzuiwa kudahili wanafunzi kwa mwaka wa masomo wa 2016/2017, Diwiz alisema ukaguzi mbalimbali ulifanywa na mamlaka mbalimbali ikiwemo TCU katika kuhakiki ubora wa elimu unaotolewa chuoni hapo na kusema ni imani yake kwamba mamlaka hizo zimeridhika na hali ilivyo.
Kwa upande wake Msika alisema ingawa tayari wanafunzi wamepewa taarifa za chuo chao kuzuiwa kufanya udahili katika mwaka huu wa masomo, bado wanasubiri taarifa zaidi kutoka serikalini juu ya jambo hilo. Hata hivyo alisema hatua hiyo itaboresha zaidi mazingira ya utolewaji wa elimu katika chuo hicho.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, alisema taarifa kamili ya kile kilichobainika kama kasoro kutokana na ukaguzi uliofanywa na Tume hiyo Maalumu kwa vyuo vya elimu ya juu itatolewa ili kasoro hizo zifahamike na kuviwezesha vyuo husika kurekebisha mapungufu yaliyobainika. Alisema mkakati wa Serikali ya Awamu ya Tano tangu ilipoingia madarakani ni kuhakikisha kuwa nchi inazalisha wasomi wenye sifa.
JIUNGE NASI , BONYEZA HAPA http://www.wabunifumedia.blogspot.com ku-install App ya wabunifumedia, bila ya kuingia website
Tweet@wabunifumediaonline, youtube@wabunifumediaonline TV, Fb@wabunifumediaonline, insta@wabunifumediaonline
JIUNGE NASI , BONYEZA HAPA http://www.wabunifumedia.blogspot.com ku-install App ya wabunifumedia, bila ya kuingia website
Tweet@wabunifumediaonline, youtube@wabunifumediaonline TV, Fb@wabunifumediaonline, insta@wabunifumediaonline
Tweet@wabunifumediaonline, youtube@wabunifumediaonline TV, Fb@wabunifumediaonline, insta@wabunifumediaonline
Post a Comment