Na Odrian Nicolaus, WM (TSJ)
UKOSEFU wa daraja katika
bonde la mto Mzumbi unaonganisha mtaa wa Mgeule Juu kata ya Buyuni na maeneo
mengine ya manispaa ya Ilala Jijini Dar es Salaam imetajwa kuwa chanzo cha
kusuasua kwa maendeleo ya elimu na uchumi katika mtaa huo.
Bonde la mto Mzumbi unaonganisha mtaa wa Mgeule Juu kata ya Buyuni na maeneo mengine ya manispaa ya Ilala Jijini Dar es Salaam |
Wakizungumza na
waandishi wa habari waliokuwa kwenye ziara ya kikazi ya kutembelea miradi ya
maendeleo mtaani humo hivi karibuni, baadhi ya wakazi wa eneo hilo walisema
wanafunzi wamekuwa wakikatisha masomo msimu wote wa mvua kwa kushindwa kuvuka
mto huo kwenda shule.
Mmoja wa wakazi hao, Anastazia
Marandu alisema kutokana na eneo hilo kutokuwa na shule ya msingi na sekondari
inawalazimu wanafunzi kutembea umbali wa kilometa nne huku wakilazimika kuvuka
mto huo ambao hujaa msimu wa mvua.
“Maji hujaa na kufikia
kimo cha mita mbili hadi mbili na nusu kwenda juu. Huwalazimu watoto kutokwenda
shule, hadi msimu umalizike. Ikumbukwe
kwamba hakuna njia mbadala. Ni muhimu kuwa na daraja mahala hapa,”alisema.
Naye Salum Tupa aliongeza kwa kusema kuwa
shughuli nyingine kama vile biashara pia hukwama wakati wa msimu hata kama
msimu huo utadumu kwa mvua kwa miezi mitatu mfululizo.
“Wakati mwingine kama
hukununua chakula cha kutosha ndani, lazima usaidiwe na majirani. Mto huanzia
Morogoro kupitia Kisarawe mkoani Pwani, hivyo maji yake hujaa na kuchukua muda
mrefu kupungua au kukauka, kusababisha watu kushindwa kuvuka upande wa pili wa
Buyuni CCM ambako tunapata mahitaji,”alisema.
Mjumbe wa kamati ya
maendeleo ya serikali ya mtaa huo, Baraka Koka alisema uongozi wa mtaa huo
ulifikisha kero hiyo kwa Diwani wa kata hiyo na kuahidi kulijadili kwenye kamati
ya maendeleo ya kata (WDC) ili maamuzi hayo yafikishwe kwa Mkurugenzi wa
Manispaa kwa lengo la kupata kivuko au daraja.
“Sina hakika kama suala
hili lilijadiliwa na ngazi ya juu na ufumbuzi wake ni nini kwasababu hakuna
juhudi zozote zinazonekana kumaliza kero hii,”alisema,
Akifafanua kuhusu kero
hizo, Mkuu wa wilaya ya Ilala, Sophia Mjema alisema serikali wilayani humo
imeanza hatua za kuyabaini maeneo yenye kero mbalimbali ikiwamo pembezoni mwa Ilala.
Kutokana na
hayo Bi Sophia aliwaomba wananchi wa wilaya yake ya Ilala. Kuwa
wavumilivu wakati wakiyafanyia kazi matatizo yanayowakabili katika maeneo.
Katika ziara hiyo ya
waandishi wa habari wa taasisi ya kihabari ya Wabunifu (WM) na ile ya waandishi
wa habari za uwazi na uchunguzi, Sauti ya Wasiokuwa na Sauti Vijijini (TTAJA)
walibaini barabara kuu ya kuingia mtaa huo ikiwa na mashimo ya kutisha huku
daraja la kienyeji lililojengwa kwa magogo ya mti wa mnazi likiwa limesombwa na
maji na hivyo kukosekana kwa mawasiliano kati ya wananchi hao na maeneo mengine
ya jijini.
JIUNGE NASI , BONYEZA HAPA http://www.wabunifumedia.blogspot.com ku-install App ya wabunifumedia, bila ya kuingia website
Tweet@wabunifumediaonline, youtube@wabunifumediaonline TV, Fb@wabunifumediaonline, insta@wabunifumediaonline
Tweet@wabunifumediaonline, youtube@wabunifumediaonline TV, Fb@wabunifumediaonline, insta@wabunifumediaonline
Post a Comment