Na Odriani Nicolaus, TSJ.
WAKAZI wa mtaa wa Mgeule, Kata ya Buyuni, Manispaa ya Ilala nje kidogo ya Jiji La Dar es Salaam, wameiomba halmashauri ya Manispaa hiyo kujenga daraja litakalounganisha eneo hilo na maeneo mengine ya jiji ili kuwa na uhakika wa mawasiliano kwao wakati wa mvua.
Wakizungumza na timu ya waandishi wa habari
waliotembelea miradi ya maendeleo katika maeneo ya pembezoni mwa Manispaa ya
Ilala, walisema kukosekana kwa daraja hilo imekuwa chanzo cha maendeleo duni ya
uchumi kutokana shughuli za kibiashara kukwama.
Mmoja wakazi hao Bruno Benard Ndege alisema pia kadhia hiyo
imechangia kushuka kwa kiwango cha elimu kutokana na wanafunzi wengi wa
mtaa huo na ule wa Mgeule Juu kushindwa kwenda shule karibu kipindi chote cha
msimu wa mvua.
“Tunashukuru juhudi za viongozi wetu wa mtaa,
wamekuwa wakifanya kila njia kuondoa tatizo hili, lakini lazima kuwapo kwa
suluhisho la kudumu kutoka serikalini hasa katika bajeti ya Manispaa,”alisema Ndege.
Ndege ambaye pia ni mjumbe wa shina katika eneo
hilo, aliongeza kwa kusema kuwa ujenzi wa daraja hilo ni jambo mtambuka
kutokana na matumizi ya barabara kuu ya kutoka eneo la Kwa Mbiki hadi Mgeule
juu kutumiwa na zaidi ya mtaa mmoja katika shughuli za maendeleo na kibinadamu.
Mkazi mwingine, Nurdin Shemtanduloo alisema kutokuwepo kwa daraja hilo kunaweza
kuathiri mpango wa serikali ya mtaa huo wa ujenzi wa soko kutokana na ukweli
kwamba wafanyabishara wengi watashidwa kusafirisha bidhaa zao.
“Ujenzi wa daraja hili utasaidia kwenda na kasi ya
sasa wa kufanya kazi kwa bidii, biashara na shughuli nyingine kama hizo za
kupunguza au kumaliza kabisa umasikini,”alisema.
Naye Elizabeth Mwakapangala, alisema wanawake wengi
wajawazito wamekuwa kwenye hatari zaidi wakati wa msimu wa mvua kutokana na
kushindwa kufika hospitali ya wilaya ya Ilala, Amana, kwa ajili ya kujifungua au zahanati ya Buyuni
kushiriki kliniki.
“Wakati wa msimu wa mvua hali ya mama wajazito
tunakuwa kwenye hatari zaidi kwasababu hakuna njia ya kupita, huweza kuwalazimu
wanawake wengi kujifungulia nyumbani jambo ambalo ni hatari sana kwa afya ya
mama na mtoto”alisema.
Zaidi, aliongeza kuwa ipo haja ya kuharakishwa kwa
mchakato wa ujenzi wa zahanati kwenye mtaa huo na kuiomba serikali kusaidia
juhudi za viongozi wa mtaa wao katika mpango wa kujenga zahanati ili kupunguza
vifo vya mama na watoto ambao kwasbabu za kibiolojia kundi la mama wajawazito
na watoto chini ya miaka mitano hufa zaidi kwa ugonjwa wa malaria na matatizo
ya uzazi.
“Kuna watu wanaozuia huu mpango na eneo letu la
zahanati, wajawazito na wanawake wengine tumeapa ipo siku tutawalaani hadharani
na hakika tutamwaga razi mbele yao ili waone tumechoka na kero hii ya kukosa
zahanati na maumivu ya uchungu hadi Amana au Buyuni,” alikasirika Mwakapangala.
Mjumbe wa
kamati ya Maendeleo ya Mtaa huo, Maliki Shemtandulo alisema uongozi wa mtaa
umewasilisha kero hiyo kwenye mamlaka serikali ingawa michango na juhudi za
wananchi ni muhimu kufanikisha kero mbalimbali za mtaa huo.Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Mgeule, John Lazaro Mwatebela alisema kero ya daraja imewasilishwa kwa Mhandisi wa Manispaa ya Ilala na ameahidi kuingiza katika bajeti ya Manispaa katika mwaka huu wa fedha.
“Juhudi zetu kama jamii kwa sasa ni kupunguza upana wa mto kwa kujaza kifusi
ili kurahisisha ujenzi huo mara
utakapoanza ambapo, katika mazungumzo yetu na mhandisi alituahidi kwamba kabla
ya Julai mwaka huu wataanza ujenzi baada ya upembuzi yakinifu
kukamilika,”alisema.
Mtaa wa Mgeule ni mojawapo ya mitaa nane ya Kata ya
Buyuni inayokabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo, maji safi, soko, umeme, zahanati
na uhaba wa walimu katika shule mpya ya msingi Mgeule yenye walimu 14
wanaohudumia wanafuzi zaidi 700.
Kwa mujibu wa sera ya elimu ya mwaka 2003, mwalimu
mmoja anatakiwa kuhudumia wanafunzi 45 katika chumba kimoja cha darasa hivyo kufanya shule hiyo kwa sasa kuwa na
hitaji la walimu 16 sawa na hitaji la walimu wawili zaidi.
JIUNGE NASI , BONYEZA HAPA http://www.wabunifumedia.blogspot.com ku-install App ya wabunifumedia, bila ya kuingia website
Tweet@wabunifumediaonline, youtube@wabunifumediaonline TV, Fb@wabunifumediaonline, insta@wabunifumediaonline
Tweet@wabunifumediaonline, youtube@wabunifumediaonline TV, Fb@wabunifumediaonline, insta@wabunifumediaonline
Post a Comment