BAADHI ya wakazi wa mtaa wa Mgeule Kata ya Buyuni katika Manispaa ya Ilala nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, wamedai kukosa huduma muhimu za kijamii kutokana na kukosekana kwa usawa na vipaumbele katika mgawanyo fedha za miradi ya maendeleo za mfuko wa jimbo la Ukonga.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na timu ya waandishi wa habari wa taasisi ya habari ya Wabunifu (WM) ya jijini humo, wakazi hao wamemlaumu Diwani wa kata hiyo Twaha Malate (CCM) kupendelea baadhi ya maeneo katika kutekeleza miradi ya maendeleo kwa fedha za mfuko huo.
“Tunaishukuru Manispaa na mkoa kwa ujumla wameona juhudi zetu na kuongeza madarasa kutoka darasa moja tulilojenga kwa nguvu zetu na sasa shule ina madarasa 13 na madawati ya kutosha…lakini hatujafaidika na fedha za mfuko wa jimbo tangu diwani achaguliwe,”alisema mmoja, Elizabert Mwakapangala.
Badala yake fedha nyingi za Kata hiyo kutoka mfuko wa jimbo zimekuwa zikielekezwa zaidi kutekeleza miradi ya maendeleo katika mitaa ya Taliani na Nyeburu kwa kile kilichodaiwa kuwa wananchi wa maeneo hayo walimchagua Diwani huyo kwa kura nyingi na kwamba kitendo cha kuelekeza miradi mingi huko ni kuwapa fadhila.
Waandishi wa habari wa WM wakiwa kwenye eneo la ujenzi wa zahanati ya mtaa huo ambapo pia walishuhudia kituo cha mama na mtoto (PICHA: ETHAN MBUYA). |
Meneja Miradi wa WM na Mwenyekiti Mtendaji wa TTAJA, Moris Lyimo (aliyesimama katikati) akifafanua jambo kwa wafanyakazi wenzake kabla ya kuanza kwa ziara ya kutembelea miradi ya maendeleo katika mtaa wa Mgeule, Kata ya Buyuni, Manispaa ya Ilala Jijini Dar es Salaam hivi karibuni (PICHA: ETHAN MBUYA). |
Mwananchi mwingine, Baraka Koka alisema eneo hilo lina kila sababu ya kupewa kipaumbele kutika fedha za mfumo wa jimbo kutokana na adha ya mafuriko wakati wa msimu wa mvua kwa kukosa daraja na kusababisha mahudhurio yasiyoridhisha kwa wanafunzi na shughuli nyingine za kijamii.
“Hapa kwetu kuna mabonde yanayoweza kuvukika msimu wa mvua kwa kujenga madaraja tu, fedha za jimbo zinatolewa kwenye kata lakini hatuoni kipaumbele hiki kikitekelezwa japokuwa ni huduma mtambuka,”alisema Koka.
Baadhi ya majengo ya shule ya msingi Mgeule ambayo sehemu yake imejengwa kwa nguvu za wananchi wa mtaa huo, uliopo kata ya Buyuni, Manispaa ya Ilala jijini Dar es Salaam. Kwa sasa shule hii iliyojengwa kwa muda wa mwaka mmoja ina wanafunzi zaidi ya 700 (PICHA: ETHAN MBUYA). |
Sehemu ya wananchi wa mtaa wa Mgeule katika mkutano na waandishi wa habari wa WM walipotembelea mtaa huo hivi karibuni (PICHA: ETHAN MBUYA).
Naye Mwenyekiti wa mtaa huo, John Lazaro Mwatebela alisema kuwa juhudi za pamoja zinahitajika katika kutekeleza Ilani ya CCM kwa kuangalia vipaumbele kulingana na ukubwa wa kero katika dhana ya kutekeleza kwa vitendo kauli mbiu ya `Hapa Kazi Tu’.
Alikiri eneo hilo kukabiliwa na kero kadhaa ingawa baadhi zimepunguzwa kwa juhudi binafsi, nguvu za wananchi na Manispaa.
“Tunashukuru juhudi za serikali hasa Manispaa ya Ilala kwa kuuunga mkono juhudi zinazoanzishwa na wananchi, ingawa nguvu ya serikali inahitajika zaidi katika kutatua kero nyingine ufumbuzi wake umeanza kwa sisi kubuni namna ya kukabiliana nazo,”alisema.
Kwa upande Diwani Malate alikanusha tuhuma hizo kwa madai kuwa amehusika katika ujenzi wa shule moja kwenye mtaa huo kwa idadi ya madarasa nane.
"Madai yao sio ya kweli. Huo mtaa wa Nyeburu wanaousema sijafanya chochote, ila kinachofanyika pale ni kwamba Mwenyekiti wa mtaa huo (Nyeburu) anatumia pesa zake mwenyewe sasa watu wakiona tingatinga linachonga barabara wanajua mimi ndiye ninafanya," alisema na kuongeza …
"Wananchi kulalamika ni haki yao kwani kata yangu ina mitaa 8 ni kubwa mno, sijawahi kupata mradi hata mmoja... bajeti ni ndogo ingawa naendelea kufatilia, ninawaomba wawe na subra, hakuna kero ambayo haitatatuliwa," alisema Malate.
=================
JIUNGE NASI , BONYEZA HAPA http://www.wabunifumedia.blogspot.com ku-install App ya wabunifumedia, bila ya kuingia websiteTweet@wabunifumediaonline, youtube@wabunifumediaonline TV, Fb@wabunifumediaonline, insta@wabunifumediaonline
Post a Comment