Mgeule walilia huduma ya maji safi
Na.Mwanaidi Mziray
WAKAZI wa mitaa ya Mgeule na Mgeule Juu, Kata ya Buyuni Manispaa ya Ilala nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam wapo hatarini kupatwa na magonjwa ya kuambukiza kutokana na maeneo hayo kutokuwa na huduma ya maji safi na salama.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na timu ya waandishi wa habari wa taasisi ya habari ya Wabunifu (WM) ya jijini humo baadhi ya wakazi hao walisema kwa kipindi chote cha maisha hayo wamekuwa wakilazimika kutumia maji ya visima vilivyochimbwa kwenye mabonde yanayozunguka eneo hilo ambayo sio salama kutokana na ongezeko la watu.
Mmoja wa wakazi wa mtaa wa Mgule, Elizabert Mwakapangala alisema kero hiyo imekuwa adha kwa wanawake na watoto kutokana na kutumia muda mwingi kutafuta maji maeneo ya mbali hasa wakati wa kiangazi ambapo visima hivyo hukauka au kuwa na maji machache ambayo hayakidhi mahitaji ya watu.
"Tunamshukuru sana Mwenyekiti wetu wa mtaa na kamati yake ya maendeleo kutokana na juhudi zao ambazo zimesaidia kupatikana kwa miradi miwili ya visima virefu vya maji, lakini jambo la kustaajabisha ni miradi hiyo kusuasua licha ya kazi ya uchimbaji kumalizika,"alisema.
Alisema wanachofahamu ni kwamba uchimbaji wa visima hivyo ulikamilika mwaka mmoja uliopita na kuahidiwa kwamba hatua ambayo ingefuata mara moja ni utandazaji mabomba na uwekaji wa vituo vya maji, lakini hadi sasa kazi hizo hazijafanyika.
Naye Baraka Koka alisema katika mtaa wa Mgeule Juu hali ni mbaya zaidi kutokana na jiografia ya eneo hilo kuwa mbali na barabara kuu ya Chanika ambako huduma ya maji safi hupatikana.
"Kama hapa Mgeule wanaungua, sisi huko Mgeule Juu tunataketea...tunaweza kupata kipindupindu kwani hata maji tunayotumia ni kama malambo, hayajapimwa tofauti na wenzetu wa hapa Mgeule ambao hutumia visima vya zege ambayo kimsingi yamekingwa hata angalau kutofikiwa au kuingia wadudu kwa urahisi,"alisema Koka.
Mjumbe wa Kamati ya Maendeleo ya mtaa Mgeule, Maliki Shemtandulo alikiri mtaa huo kuwa kero ya maji kwa muda mrefu ingawa juhudi za kukabiliana na kadhia hiyo zinaendelea kati ya mtaa na mamlaka serikalini.
Mwenyekiti wa mtaa huo John Mwatebela alisema kamati ya maendeleo ya mtaa huo imefanikiwa kukutana na uongozi wa Manispaa ya Ilala na Mamlaka ya Maji Safi Dar es Salaam (Dawasa) ambapo kwa upande wa Manispaa walikubali ombi la kumaliza kero hiyo kwa kuchimba kisima kirefu cha mita 180.
"Wakati Manispaa ikichimba kisima hicho eneo la Mianzini, Dawasa wao walichimba cha urefu wa zaidi ya mita 600. Ni kweli kwamba uchimbaji wa visima vyote viwili ulikamilika zaidi ya mwaka mmoja uliopita na waliahidi kuja kuweka mabomba ambapo wananchi walikubali kutoa maeneo yao, hata mimi nashangaa kwanini hadi sasa hawajarudi,"alisema Mwatebela.
Hata hivyo aliffafanua kuwa uongozi wa mtaa ulifuatilia ambapo kwa upande wa Manispaa ya Ilala uliahidi kuingiza katika bajeti ya 2016/2017 mpango wa usambazaji wa mabomba kutokana na bajeti ya mwaka ulipiota kuwa finyu.
"Kwa upande wa mradi wa Dawasa, sisi tumetekeleza hatua zote ikiwa ni pamoja na kufanya matayarisho ya takwa la Wizara ya Maji la kuunda Jumuiya za Watua Maji ambapo kamati ingepaswa kuundwa mara tu baada ya mtaa kubabishiwa mradi, jambo la kushangaza ni wao kuja kutoa vifaa, na kuchukua mchanga eti kwa ajili ya upimaji, hata sisi tulishikwa na butwaa,"alishangaa Mwatebela.
Mwandishi alipiga hodi ofisi ya Dawasa makao makuu na Manispaa ya Ilala ambapo kwa nyakati tofauti hakufanikiwa kukutana na wahusika kufafanua sintofahamu kuhusu miradi hiyo kwa kile kilichodaiwa na wasiohusika kuwa wahusika wako kwenye mkutano na wakati mwingine alijibiwa kuwa wako nje ya ofisi.
JIUNGE NASI , BONYEZA HAPA http://www.wabunifumedia.blogspot.com ku-install App ya wabunifumedia, bila ya kuingia website
Tweet@wabunifumediaonline, youtube@wabunifumediaonline TV, Fb@wabunifumediaonline, insta@wabunifumediaonline
Post a Comment