Na Yusuph Mwamba
BEKI wa klabu ya soka ya Simba, Method Mwanjale amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa Desemba wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa msimu wa mwaka 2016/2017.
Beki huyo wa kati, aliwashinda kiungo mshambuliaji wa Yanga, Haruna Niyonzima na beki Yakubu Mohamed wa Azam FC.
Mwezi Desemba ulichezwa raundi tatu za ligi hiyo, huku Simba ikicheza mechi mbili ugenini na moja nyumbani. Raundi hizo ni ya 16, 17 na 18.
Mwanjali aliiongoza Simba kushinda mechi zote tatu, hivyo timu yake kupata ushindi wa asilimia 100 kwa kunyakua pointi zote tisa, na kubaki katika nafasi yao ya kwanza kwenye msimamo wa Ligi, nafasi ambayo walikuwa nayo wakati wanaingia raundi ya 16.
Pia katika raundi hizo tatu, ambapo Simba haikufungwa bao hata moja, Mwanjali alicheza dakika zote 270, na bila kuoneshwa kadi yoyote.
Taarifa hiyo ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) inasema kuwa mchezaji huyo alichangia kwa kiasi kikubwa katika mafanikio ya timu yake, ambapo aliongoza safu ya ulinzi.
Kwa kushinda tuzo hiyo ya mchezaji bora, Mwanjali atazawadiwa kitita cha Sh milioni 1 na wadhamini wakuu wa ligi hiyo, ambao ni Kampuni ya Simu za Mkononi ya Vodacom Tanzania.
Wachezaji wengine walioshinda tuzo za mchezaji bora kwa msimu wa 2016/2017 hadi sasa ni John Bocco wa Azam (Agosti), Shiza Ramadhan Kichuya wa Simba (Septemba), Simon Happygod Msuva wa Yanga (Oktoba) na Rifati Hamisi wa Ndanda (Novemba).
JIUNGE NASI , BONYEZA HAPA http://www.wabunifumedia.blogspot.com ku-install App ya wabunifumedia, bila ya kuingia websiteTweet@wabunifumediaonline, youtube@wabunifumediaonline TV, Fb@wabunifumediaonline, insta@wabunifumediaonline
Post a Comment