TIMU
ya Azam FC wanalamba lamba , usiku wa Jumatano imeichapa Ashanti United mabao 4-0,
katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa Azam Complex.
Mchezo
huo ulikuwa ni mahususi kwa ajili ya kuwaweka kwenye ushindani
wachezaji, pia wakipasha misuli kuelekea mchezo ujao wa Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Ruvu Shooting utakaofanyika uwanja
huo Jumamosi hii saa 1.00 usiku.
Azam
FC ilifanikiwa kutawala vipindi vyote vya mchezo huo, huku benchi la
ufundi likichezesha vikosi viwili tofauti katika kila kipindi cha mchezo
huo, isipokuwa wachezaji wawili beki wa kulia, Swaleh Abdallah na
kiungo Masoud Abdallah, ambao ni majeruhi.
Mabingwa
hao wa Kombe la Mapinduzi na Ngao ya Jamii msimu uliopita walijipatia
mabao mawili katika kila kipindi, ambapo winga Enock Atta Agyei,
aliyeendelea kuwa kwenye kiwango chake kizuri alifunga bao la uongozi
dakika ya nane baada ya kuitoka safu ya ulinzi ya Ashanti na kupiga
shuti lililojaa wavuni.
Winga
Idd Kipagwile, alipigilia msumari wa pili dakika ya 31 baada ya kuingia
kwa kasi kwenye eneo la 18 la Ashanti na kupiga shuti lililomshinda
kipa na hivyo kufanya dakika 45 za kipindi cha kwanza kumalizika kwa
uongozi wa mabao mawili ya Azam FC huku Ashanti wakiwa hawajapata kitu.
Kipindi
cha pili Azam FC ilihitimisha ushindi huo mnono kwa mabao mengine
mawili, yaliyofungwa na mshambuliaji Wazir Junior dakika ya 75 na
jingine likiwekwa kimiani kwa mkwaju wa penalti na beki David Mwantika
dakika ya 86.
Kiungo Salmin Hoza, angeweza kuipatia mabao mengine mawili Azam FC baada ya mashuti yake mawili aliyopiga kugonga mwamba.
Mara
baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kimeingia moja kwa moja kambini
kujiandaa na mchezo ujao wa ligi dhidi ya Ruvu Shooting, utakaofanyika
wikiendi hii.
Kikosi
cha Azam FC kilikuwa; Razak Abalora/Mwadini Ally dk 46, Daniel
Amoah/Joseph Mahundi dk 46, Bruce Kangwa/Braison Raphael dk 46, Aggrey
Moris/David Mwantika dk 46, Yakubu Mohammed/Abdallah Kheri dk 46, Himid
Mao (C)/Stephan Kingue dk 46, Salum Abubakar/Salmin Hoza dk 46, Idd
Kipagwile/Frank Domayo dk 46, Mbaraka Yusuph/Yahaya Mohammed dk
46/Kangwa dk 72, Yahya Zayd/Wazir Junior dk 46, Enock Atta/Ramadhan
Singano dk 46

Post a Comment