Halloween party ideas 2015
Image

MAMBO YAKUFANYA KUELEKEA FUNGA ZA MWISHO WA MWEZI MTUKUFU WA RAMDHAN KAREEM.

Na Yusuph Mwamba.

Huku zikiwa zimebakia siku chache ya kuuaga Mwezi mtukufu wa Ramadhan Kareem, tayari kuna maagizo mbalimbali yamekuwa yakisisitiziwa na wana dhuoni wetu kutoka kwa Mwenyezi Mungu katika hizi siku mbili za mwisho wa funga ya Ramadhani haswa zaidi tukijikita kwenye swala la Zakatul Fitri.

ZAKA YA BAADA YA RAMADHANI

Huitwa Zakatu-l-fi'tri, kwa vile inapasa kutolewa kwa ajili ya Idi Alfi'tri. Pia huitwa , Zakatu-l-abdaani, (Zaka ya viwiliwili), kwa vile hutolewa kutakasa kiwiliwili na kukuza a'amali zake. Asili ya kuwajibika Zaka hii ni kwa vile walivyoeleza Al Sheikhan r.a. kutoka kwa Ibni 'Umar r.a.:
"Mtume s.a.w. amefaridhisha Zaka ya Idi-l-fi'tri juu ya kila Muislam, pishi ya tende, au pishi ya ngano; kwa kila mtu, mwanamume au mwanamke, mtoto mdogo au mtumzima".

Shuruti za Kuwajibika Kutoa Zaka ya Idi-l-Fi'tri

Shuruti za kuwajibika kutoa Zaka ya Idi-l-fi'tri ni tatu:



SHURUTI YA KWANZA
Uislam, hatoi Zaka asiekuwa Muislam.

SHURUTI YA PILI.
kutua jua kuamkia siku ya Idi; kwani hapo ndio unaingia wakati wa Idi Alfi'tri. Na qauli nyengine kuwa hutolewa kwa kuingia alfajiri ya siku ya kwanza ya Idi-l-fi'tri, hivi ni kwa vile Zaka hii ina khusiana na Idi, kwa hivyo haiitangulii Idi, kama vile inavyojuzu kufanywa kwa Zaka ya Idi-l-adh-ha.

SHURUTI YA TATU.
kuwa na uwezo; asiyekuwa na uwezo halazimiki kutoa Zaka. Uwezo ni kuwa na chakula ziada ya chakula cha kumtosha yeye mwenyewe na kila anaemlazim yeye chakula chake - ikiwa ni binaadam au wengineo - katika usiku wa kuamkia Idi na hii siku ya Idi. Zaka hutoa mtu kujitolea nafsi yake, na kila yule ambae inamlazim juu yake yeye maisha yake ya kila siku, kama vile mke wake, watoto wake, mama yake, baba yake, ndugu yake, kaka yake, dada yake, na kila yule mwenye kumtegemea yeye - ikiwa anaishi nae au haishi nae - lakini inamlazimikia juu yake yeye maisha yake ya kila siku. Mtumishi wa nyumbani Muislam na yeye vilevile hutolewa Zaka, lakini basi; ikiwa utumishi wake ni kwa malipo - mshahara - basi Zaka yake itamlazim ajitolee yeye mwenyewe.



Msingi wa Hukmu

Hatowi Zaka asiekuwa Muislam
Hapewei Zaka asiekuwa Muislam
Analazimika kutowa Zaka mwenye uwezo
Halazimiki kutowa Zaka asiekuwa na uwezo
Inalazimika kutolewa Zaka asiekuwa na uwezo
Hailazimiki kutolewea Zaka mwenye uwezo.



Kiwango cha Zaka chenye kutolewa ni pishi ya chakula cha kawaida cha nchi. Inajuzu kutoa Zaka ya Idi-l-fi'tri kwa kila kile ambacho kinajuzu kutolewa Zaka kwa kipimo cha sehemu moja ya sehemu kumi, kama vile chembechembe na mazao. Pia hujuzu kutoa Zaka maziwa ya kugandishwa (maziwa ya kuganda).

Ikiwa hicho ndio chakula chake cha kawaida huyo mwenye kutoa hio Zaka; ikiwa hicho si chakula chake cha kawaida basi haijuzu yeye kutoa Zaka kwa hicho. Na inashurutishwa kuwa chenye kutolewa kwa ajili ya Zaka kisiwe na aibu, na kiwe ni cha chembechembe; kwani hivyo ndivyo ilivyokuja kwenye Hadithi ya Mtume s.a.w. iliotaja suala hili la Zaka ya Idi-l-fi'tri, hivi ni kwamba haijuzu kutoa thamani ya hicho cha kutolewa, bali nikutolewa kama ilivyokuja kwenye Hadithi yenyewe. Ilivyokuja kwenye Hadithi ni kwamba iwe ni chakula chenye kutumika aghlab katika hio nchi, hivi ni kwa sababu faqiri hutamani na yeye apate chakula hicho.

Kwa kipimo cha Misri, pishi ni sawa na robo “kaila”; hichi hutosheleza kwa chakula cha watu wane. Kipimo kinachotumika nchi nyingi siku hizi ni thamani ya kilo (kilogram) moja ya chakula cha dasturi. Hivi huingia kama vile mchele, kitoweo na viungo vyake vya lazima. Wanazuoni wengine wamejuzisha kutoa thamani yake, ikiwa hivyo ni faida zaidi kwa hao wenye kustahiki kupewa, hivi ni kwa qauli ya Sayyidna Mu'adh r.a. kwa watu wa Yaman:
"Leteni nguo mpya au zilizovaliwa badala ya ngano na dhura (dhura ni miongoni mwa aina za ngano), kwani hivyo ni wepesi kwenu na ni kheri kwa Sahaba zake Mtume s.a.w. na kwa wakaazi wa Madina".

Hivi kusema: "….badala ya ngano na dhura…", ni dalili ya kujuzu kutoa thamani yake ikiwa hivyo ni faida zaidi kwa mafaqiri wenye kustahiki kupewe hio Zaka ya Idi-l-fi'tri. Wala haijuzu Zaka hii mtu kuwapa wazee wake, baba au mama au bibi au babu au kuwapa wajukuu zake, kwani hawa ikiwa wao hawana uwezo huwa ni juu yake yeye (mwenye kutoa Zaka) kuwaqim madam watakuwa hawana mtu mwengine wa kuwaqim isipokuwa yeye tu. Imam Maalik r.a. yeye anajuzisha mtu kutoa Zaka yake na kumpa babu, au mjukuu. Pia kwa Imam Maalik r.a. inajuzu kuwapa ndugu wa kike, ndugu wanawake wa mama, mashangazi na watoto wao, hupewa kwa sifa ya kuwa ni mafaqiri.

Haijuzu hii Zaka kusafirishwa kutoka mji kupelekwa mji mwengine, hivi ni kwa qauli ya Mtume s.a.w.: " Hadithi hii imetangulia kutajwa.

Qauli nyengine ni kwamba inajuzu hii Zaka kusafirishwa kutoka mji kupelekwa mji mwengine, hoja ya kujuzu ni hii qauli ya Mua'adhi r.a.: 

Suala hili la kujuzu au kutojuzu Zaka kupelekwa kutolewa mji mwengine, mbali na mji iliokusanywa hio Zaka, limetangulia kutajwa kwenye mlango wa matumizi ya Zaka. Ikiwa faqiri anadaiwa, ikawa yule mwenye kudai akasema kumwambia yule mwenye kudaiwa: "Nimejaalia ninachokudai kuwa ni Zaka yangu". Haitajuzu kutoa Zaka huko mpaka yule faqiri wa kupewa hio zaka aipokee hio Zaka mkononi mwake mwenyewe. Hivi ni kwa qauli ya Mtume s.a.w.:   "Watoshelezesheni wasiombe katika siku hii ".
Ama ikiwa hilo ni deni la amana, basi inajuzu kutoa Zaka kwa namna hio.

Wakati wa Kutowa Zaka ya Idi-l-Fi'tri

Ni haraam kuakhirisha kuitoa hii Zaka ila kwa 'udhru, kama vile akikosekana mwenye kustahiki kupewa, au yuko wa kupewa lakini hajaweza kumfikia kwa sababu yoyote ile. Ni afadhali kuitoa Zaka hii baada ya kuingia alfajiri ya siku ya Idi na kabla ya watu kwenda msikitini kwa Sala ya Idi. Hivi ni kwa qauli ya Ibni 'Umar r.a.:   "Na ni thawabu zaidi kutolewa kabla ya watu kwenda msikitini". (Wamekubaliana Wanazuoni wa Hadithi).
Wamekubaliana wanazuoni kujuzu kutolewa Zaka hii siku moja, au siku mbili kabla ya Idi. Abu Hanifa r.a. amejuzisha kutolewa Zaka hii hata kabla ya kuingia Ramadhani, na Imam Shafi'ii r.a. amejuzisha kutolewa Zaka hii hata awali ya Ramadhani. Na inapendekezwa Zaka hii mtu kuwapa watu wake wa karibu, yaani jamaa zake ambao halazimiki yeye kuwaqim, lakini ni wahitaji; kama vile kuwapa mama-wa-dogo, ma'ami, wajomba, mashangazi, na watoto wao, muhim iwe ni wenye kuhitaji, si wenye uwezo wao wenyewe. Kama tulivyosema mwanzo, Zaka miongoni mwa makusudio yake ni kujenga mapenzi na mawasiliano, khasa baina ya jamaa.

HIKMA YA ZAKATU-L-F'TRI


Hikma ya kufaridhishwa Zaka ya Idi-l-fi'tri ni vile Mwenyezi Mungu Mtukufu katika kutaka kum'tahirisha mja wake - baada ya kukamilisha saumu yake - kutokana na uchafu wa maneno machafu na yale ya upuuzi yaliompitia, vitendo ambavyo vimekatazwa khaasa kwa aliomo kwenye Saumu. Hivi ni kwa qauli ya Ibni 'Abbaas r.a.:

"Mtume s.a.w. amefaridhisha Zaka ya Idi-l-fi'tri ili iwe ni cha kumsafisha aliekuwa katika Saumu kutokana na uchafu wa maneno maovu na ya upuuzi". (Imehadithiwa na Abu Daud).

Vilevile hikma ya Zaka hii ni kuwaepusha ndugu zetu mafiqiri na idhlali ya kupita wakiomba katika siku hii tukufu na ya furaha. Hivi ni kwa qauli yake Mtume s.a.w.:   "Waondoleeni kupita kuzunguka (kuomba) katika siku hii". (Imehadithiwa na Al Haakim).







Post a Comment

Theme images by Maliketh. Powered by Blogger.