Na Yusuph Mwamba
MWILI wa aliyekuwa Meya wa zamani wa Jiji la Dar es Salaam, Dk Didas Masaburi, leo utaagwa na viongozi wa kitaifa pamoja wananchi wa Jiji la Dar es Salaam kwenye Viwanja vya Karimjee, kabla ya kwenda kuzikwa katika Chuo cha ugavi na ununuzi cha IPS kilichoko Chanika wilaya ya Ilala.
Msemaji wa familia, Edson Fungo aliliambia gazeti hili jana kuwa, kwa kuwa Dk Masaburi alikuwa mwanasiasa na amewahi kushika nyadhifa mbalimbali kwenye Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikalini, familia imeona vyema watoe fursa ya kuagwa na wanasiasa wenzake pamoja na wakazi wa jiji la Dar es Salaam.
Dk Masaburi kabla ya kuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, aliwahi kuwa Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki. Wakati akiwa Meya alichaguliwa pia kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa (ALART).
Hadi mauti yanamkuta, Dk Masaburi alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Magavana wa Chuo cha IPS kilichoko Chanika nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Ni katika eneo la chuo hicho ndiko marehemu atazikwa leo. Ratiba iliyotolewa na Msemaji huyo wa familia hiyo, inaonesha kuwa saa 3.00 mwili ndio utawasili kwenye Ukumbi wa Karimjee na ibada itaanza saa 4.00 asubuhi.
Utasomwa wasifu wa marehemu na baadaye kutakuwa na neno kutoka kwenye Chama Cha Mapinduzi na viongozi wa serikali.
Shughuli ya kuaga mwili wa marehemu itaanza saa 5.00 na saa 6.30 mchana msafara kwenda Chanika utaanza. Utakapowasili kutafanyika ibada ya maziko na pia wananchi wa maeneo hayo na wanajumuiya ya IPS wataanza kuaga.
JIUNGE NASI , BONYEZA HAPA http://www.wabunifumedia.blogspot.com ku-install App ya wabunifumedia, bila ya kuingia websiteTweet@wabunifumediaonline, youtube@wabunifumediaonline TV, Fb@wabunifumediaonline, insta@wabunifumediaonline
Post a Comment